STATEHOUSE GIRLS HIGH SCHOOL
STATEHOUSE GIRLS HIGH SCHOOL logo

SHAIRI

HONGERA WALIMU WA KISWAHILI

Kikorombwe napuliza, kama refa naanzisha

Debi hili kuongoza, wangu moto kuuwasha

Wetu walimu kutuza, kwa huuo mshawasha

Siwachi kuwasifia, kazi yao maridhawa

 

Kwanza yule mahiri, Bi Mung’ara jamedari

Tamlaki na kukiri, kuwa yeye hana shari

Bi Nahya yu ngangari, kutulea yu hatari

Siwachi kuwasifia, kazi yao maridhawa

 

Kinuthia twasubiri, atufunze kihodari

Na aje tu tayari, ye tumvishe johari

Sisi katu tusiwari, Bi Debra ni fahari

Siwachi kuwasifia, kazi yao maridhawa

 

Nazidi kumsifia, Barasa mwenye ujuzi

Kwake Mola namwombea, ampe nyingi mbawazi

Kwa mia asilimia, tapata si ung’amuzi

Siwachi kuwasifia, kazi yao maridhawa

 

Tele maombi sisizi, Bi Mboya kutupa njia

Kwetu tushamaizi, katu hatutajutia

Apige Mwasame mbizi, tuzidi kumsifia

Siwachi kuwasifia, kazi yao maridhawa

 

Hadi tamati naaga, walimu wameshamiri

Mbabe yule Maraga, hino lugha mekithiri

Tusiwe sisi waoga, wanoleta tahayuri

Siwachi kuwasifia, kazi yao maridhawa

 

HEKO MWALIMU MKUU

Mola namtanguliza, ujumbe kukupatia

Huenda ikakuliza, nakuomba vumilia

Yote nakueleza, mengi umeyapitia

Heko mwalimu mkuu, heri njema kuzaliwa


Kiongozi mwenye pozi,moyoni nakufikiria

Umeshazipanda ngazi,umepiga na hatua

Walimu wanakuenzi,wanafunzi nasi pia

Heko mwalimu mkuu,heri njema kuzaliwa


Mola amekuhifadhi,miaka imesogea

Kakukinga na maradhi,ukweli mnaujua

Miaka jana yakidhi,hakika imetimia

Heko mwalimu mkuu,heri njema kuzaliwa


Siku nyingi amekupa ,kuzaliwa metimia

Malezi uliyotupa,mwalimu heko twatoa

Na mazuri umetupa,mema umetujazia

Heko mwalimu mkuu,heri njema kuzaliwa


Nikiwa katikati,nimefikia hatamu

Nitakuwa wa bahati,leo nikikusalimu

Nikiupata wakati,nitautunza kwa hamu

Heko mwalimu mkuu,heri njema kuzaliwa

 

MIHIMILI YA UFANISI

Mungu mkawini ampe mbawazi  bibi yangu kwa kunipa wosia amabo kila uchao hunijenga.Ni mlumbi na mkakamavu.Katika mojawapo ya kikoa,alitueleza kuhusu mihimili na siri ya mafanikio,nami sina budi kuwamegea japo kwa kiduchu.

Mwanzo ni bidii.Kitakachobadilisha maisha yako si ruwaza kubwa uliyo nayo,bali vitendo vidogo vidogo unavyovitenda kila siku.Ikumbukwe,aghalabu huwezi kufikia kwenye kilele cha mlima pasi na kuukwea mlima wenyewe.Tia fora kwa  utendalo.Baada ya kiza,jua litachomoza matlai.Wenyewe husema siku njema…..Huo ndio utakuwa mwanzo wako mpya baada ya kukaza kamba.

Kunukuu tu maneno ya mchezaji wa  mpira wa vikapu,JOHN WOODEN, “Uwezo wako utakufikisha kilele na pale unapotaka lakini nidhamu itakudumisha pale milele.”Niruhusu niseme hivi;wengi wa watu maarufu waliofanikiwa watakunong’onezea kuwa nidhamu ni uti wa mgongo wa mafanikio.Wawe wanafunzi wenzako,mahirimu,waliokuzidi kiumri ama pia limbukeni, kila mmoja anastahili staha.Licha ya hayo penda sana kurekebishwa na kusaili.Utajifunza mengi sana kutoka kwa walimu wenye tajriba pevu katika tasnia hii.Uliza ili usije ukateleza kwenye kinamasi cha tope.

Shauku pia ni nguzo kuu  unapoazimia chochote kile.Uchu utakuelekeza palipo malengo yako.Wengi mahasidi watataka kuzamisha ndoto zako ili utetereke kama jani lisombwalo kwenye mkondo wa maji.Lakini unapochchamaa,utapiga hatua moja mbele.Mwandishi tajika S.A.  MOHAMMED katika Tumbo Lisiloshiba anasema,”Utashi ulivimba kama mahamri  yaliyonyimwa hamira.” Hii inapaswa  kuwa dira itakayokuelekeza. Je,unafahamu kuwa  katika maandamano ya kumlazimisha  Omar Al Bashir kung’atuka mamlakani kule Sudan, binti Ala Salah alihusika pakubwa.Ni mwanafunzi wa miaka 22 tu anayesomea uhandisi lakini uchu na ukakamavu wake ni wa kupigiwa mfano.Usijidunishe.

Mwisho,huwezi katu kupata ufanisi bila ushirikiano na wenzako ama ujima jinsi  ndugu zetu watanzania wanavyopenda kuita.Kila mwanafunzi ana dosari na hakuna hata anayefahamu asilimia mia.Ndivyo alivyo binadamu eti.Hakuna mkamilifu.Vitabu vitakatifu vinasema.

Kwa wanafunzi wote wa SHULE YA WASICHANA  YA STATE HOUSE:Masomo si adha unayoipitia ila ujenzi wa jumba utakalolionea  fahari siku zako za usoni.Nidhamu zangu haziniruhusu kujitia hamnazo kwa kutowataja wanaidara wakiongozwa na mkuu wa idara Bi Mung’ara kwa ushirikiano na kujifunga vibwebwe ili kulisukuma gurudumu la  lugha yetu tunu.Sina cha kuwazawidi ila shukrani za dhati.

Kevin Were Chisaka                                                                                                                                  

Related pages

Undefined index: posterImage
An error has occurred while displaying the data

Article Guide | Journalism Policy All Rights Reserved. Copyright © STATEHOUSE GIRLS HIGH SCHOOL 2020. Powered by Elimu Holdings .

Welcome

Please pick the category that fits you best